NJIA 5 ZA KUPATA WAZO LA BIASHARA BORA
1: TAFUTA UHITAJI
Kila mafanikio ni matokeo ya
uhitaji wa watu. Kila unacholipia pesa, kwako ni UHITAJI na
kwa unayempa pesa ni kuwa AMETATUA TATIZO lako.
Kwa maneno mengine. Kadiri unavyoweza kutatua matatizo MAKUBWA
na MENGI ndivyo unavyopata vyanzo vya pesa zaidi. Kwa ufupi umaskini ni matokeo
ya kukimbia kutatua matatizo na utajiri ni matokeo ya kukimbilia kutatua
matatizo.
Leo ningependa tuangalie njia kadhaa za namna ya kupata
mawazo yanayoweza kuwa chanzo cha kubadilisha maisha yako unapoamua kuyafanyia
kazi.
Na hapa ningependa kuwakumbusha maneno ya William Cameron
aliyesema; “Money never starts an idea; it is the idea that starts the money.”
Fedha haileti mawazo ila mawazo ndiyo huleta pesa, ndiyo
maana kuna watu walishawahi kupata pesa nyingi ila kwa kukosa mawazo wamerudi
katika kufeli na umaskini.
Hebu chukua dakika moja, jiulize; Katika mazingira niliyopo,
je, kuna uhitaji gani ninaoweza kuutatua? Chukua note book yako na andika kabla
hatujaendelea.
Hivyo basi angalia mazingira yanayokuzunguka, je, kuna
uhitaji gani? Kama maji yanatoka mara moja kwa wiki mtaani kwenu, ukifanikiwa
kununua simtank kadhaa na kuuza maji siku ambazo hayatoki hapo unakuwa umetatua
tatizo na umepata pesa. Kama umegundua watu karibu na maeneo ya kwenu
wanatumia gesi na hakuna duka la karibu, tafuta namna ya kuwa wakala wa kuuza,
kadhalika na mahitaji mengine eneo ulilopo.
2: BORESHA WAZO LA MWINGINE
Kuna wakati mwingine hutahitaji kuanza na wazo jipya
kabisa, badala yake utahitaji kuchukua wazo la mwingine kuliboresha. Kwa mfano
badala ya mtu kuuza matunda na kuyamenya mtu anaponunua mwingine akaboresha
akaamua kuyamenya kabisa kisha anayapaki vizuri tayari kwa kuyauza.
Chunguza kile ambacho kinafanywa na wengine kisha jiulize,
hivi nawezaje kuliboresha wazo hili?
3: HAMISHA WAZO LA WENGINE NA LIPE UHALISIA WA MAZINGIRA
YAKO
Kuna mawazo mengi yaliyofanikiwa leo ni matokeo ya mawazo
yaliyohamishwa kutoka mahali pengine na yakapewa uhalisia wa mahali husika.
X-Factor ya Uingereza imezaa Bongo Star Search, DECA na SONY Records label
ndiyo leo tunaona WCB.
Jaribu kuangalia, kuna wazo gani ambalo unaweza kulichukua
na ukaliwekea mazingira ya kwako na ukalifanyia kazi. Unaweza kulitoa nje ya
Tanzania na ukalileta Tanzania au ukalitoa Dar na ukalipeleka katika mkoa
unaoishi.
4: RAHISISHA MCHAKATO WA KITU AMA BIDHAA FULANI.
Sasa hivi kila mtu anajitahidi kutumia teknolojia kuuza
bidhaa au kutoa huduma. Kwa nini? Kwa sababu ya kurahisisha mchakato kwa
wateja.Tunaishi katika ulimwengu ambao watu hupenda kutumia muda mfupi kupata
huduma au bidhaa, hivyo unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa hata kama
unatoa bidhaa au huduma ileile kama wengine, jaribu kurahisisha.
Ndiyo maana visimbuzi wanaweka huduma zao kwenye MPESA,
Tigopesa, Airtel n.k, wanachojaribu kufanya ni kurahisisha.
Ni rahisi kwa mama ntilie anayepeleka chakula maofisini na
akaongeza gharama ya usafiri juu ya 500 kwa kila sahani kuliko auze bei ya
chini huku akisubiri watu wamfuate kilometa moja kule anakouza.
Inawezekana unataka kufanya kitu ambacho kila mtu anafanya,
swali ni je, unaweza kutoa urahisi gani utakaovutia wanunuaji wa huduma au
bidhaa yako?
5: TENGENEZA UHITAJI
Hii si njia rahisi sana ila inawezekana. Inamaanisha kuna
vitu vingi watu wanahitaji ila hawawezi kuvitumia hadi viwepo.
Kabla soda hazijaja watu walikuwa wanakunywa maji, kabla TV
hazipo watu walikuwa ni radio tu na hakuna mtu alikuwa anadai TV kwa kuwa
haikuwepo. Lakini leo ni kama vile haiwezekani kuishi bila TV. Kuna mtu siku
moja akauliza; “Hivi wazee wa zamani waliishije bila simu? Miahadi walifanyaje
wakifika Kariakoo na kila mtu yuko kona yake?”
Hii ina maana kuna mahitaji mengi bado yako ila watu
hawawezi kuyadai au kuulizia hadi yatakapokuwepo. Zamani scrub hazikuwepo
ukienda saloon, lakini siku hizi ni kama vile ni lazima kila ukinyoa utajikuta
unataka kufanya na scrub, tena ina bei kubwa kuliko hata kunyoa kwenyewe!
Hiyo inamaanisha kuna wazo unaweza ukaja nalo watu wakaanza
kuhitaji hata kama hawajawahi kujua kama wanahitaji.
MWISHO
Nyamka
comapny ltd
www.nyamkacollection21.blogspot.com
Comments
Post a Comment