Kanuni 15 za Ujasiriamali Ambazo ni Lazima Uzifahamu!!!
Ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa ajira umekuwa wa shida
sana, watu wengi hujikuta wakiwa na chaguo la kuwa wajasiriamali pekee kwenye
maisha yao.
Wengi hutamani au hata kujiingiza kwenye ujasiriamali,
lakini siyo wote wanaofanikiwa kutokana na kutokufahamu kanuni muhimu za
ujasiriamali.
Ni wazi kuwa ili uanzishe kitu chochote chenye mafanikio, ni
lazima ufahamu kanuni za kukifanya kitu hicho jinsi ipasavyo.
Ikiwa wewe ni mjasiriamali, au unataka kuwa mjasiriamali,
basi fuatilia makala hii ili nikufahamishe kanuni 7 za ujasiriamali.
1. Kuwa mtatuzi wa matatizo
Ujasiriamali ni zaidi ya kupata pesa, ni lazima kwanza
utatue changamoto ya mtu ndipo utaweza kupata pesa kutoka kwa mtu husika.
Ni muhimu ukafahamu kanuni hii kama mjasiriamali kwani
hutojikita kutafuta pesa bali utajikita kutatua matatizo ya watu.
Kwa mfano kama kuna tatizo la upatikanaji wa mboga katika
mji au eneo unalokaa, ikiwa wewe utaleta mboga katika eneo hilo ni wazi kuwa
watu watakupa pesa ili uwape mboga.
Hivyo ni muhimu kila mara ukatafuta changamoto ukaitatua,
nawe bila shaka utapata pesa za uhakika.
“Pesa ni matokeo ya kutatua shida ya mtu”
2. Kuwa na maono
Hakuna ujasiriamali bila maono. Kuwa mjasiriamali bila maono
ni sawa na kuendesha gari isiyokuwa na usukani. Maono katika ujasiriamali
yatakuwezesha kukuongoza ufanye nini na kwa muda gani.
Ni lazima ujiulize kuwa unataka kuwa nani, lini na unataka
kufanya nini baadaye?
Jonathan Swift alisema maono ni sanaa ya kuona kile ambacho
wengine hawaoni.
Ni lazima uwe na lengo na ufanye bidii kulifikia.
“Wajasiriamali waliofanikiwa ni wale walioweza kubadili
maono yao kuwa uhalisia”
3. Chagua washirika au timu sahihi
Wakati mwingine utahitaji kufanya kazi na watu au mtu
fulani. Ni muhimu kuwa makini wakati wa kuchagua washirika au timu ya kufanya
nayo kazi ili kuhakikisha maono yako hayakwamishwi.
Kamwe usichukue mtu tu kwa kigezo kuwa ni rafiki au ndugu
yako, bali chukua mtu ambaye unaamini anaweza kufanya kitu chenye tija kwa ajili
ya kufanikisha malengo yako kama mjasiriamali.
4. Toa huduma au bidhaa yenye tija
Hivi leo sokoni kuna bidhaa na huduma nyingi ambazo ni za
aina moja, lakini siyo zote zinafanya vizuri.
Hii ni kutokana na baadhi ya bidhaa au huduma kutozingatia
kuwa na tija kwa wateja wake.
Ikiwa unatengeneza bidhaa au huduma fulani hakikisha itakuwa
na manufaa makubwa na ya uhakika kwa wateja wako.
Kwa mfano nimewahi kuona vitafunwa vilivyoandaliwa katika
mazingira duni na kuwa na dosari mbalimbali kama vile marashi, vipande vya
nywele, mchanga n.k. Ni wazi kuwa bidhaa za namna hii zitakosa wateja kutokana
na kuwa na ubora duni.
Kila mara kumbuka kuwa ushindani ni mkubwa, hivyo jitahidi
kuongeza tija na ubora wa huduma na bidhaa zako.
5. Fahamu na jali wateja
Ikiwa wewe ni mjasiriamali, basi futa mawazo kuwa wateja
wanakuhitaji wewe.
Fahamu kuwa wewe kama mjasiriamali, ndiye unaye wahitaji
wateja ili ukuze biashara au huduma yako. Hakikisha mambo haya kuhusu wateja:
Fahamu wanataka nini.
Sikiliza maoni na ushauri wao.
Hakikisha unakamilisha mahitaji yao.
Tumia lugha nzuri na rafiki kwa wateja.
Mfanye mteja aone unamthamini.
Mfanye mteja aone kuwa umetanguliza huduma kabla ya pesa.
Naamini kwa kufanya hivi utaweza kujijengea msingi mzuri wa
wateja kwa ajili ya huduma au bidhaa zako kila siku.
6. Tumia pesa vyema
Changamoto ya matumizi mabaya ya pesa inawakabili watu wengi
kuanzia kwenye matumizi yao binafsi ya pesa. Watu wengi wanapata pesa lakini
zinaisha bila ya kufahamu wamezitumiaje au wamefanya kipi chenye tija.
Ni wazi kuwa matumizi mazuri ya pesa ni kanuni muhimu sana
kwa mjasiriamali, kwani kwa njia hii utaweza kukuza biashara yako kila siku.
Jifunze kufahamu hii ni pesa kwa ajili ya nini, na uitumie kwa mambo ya msingi
pekee.
Epuka tabia za kibadhirifu na anasa. Ikiwa biashara au
uwekezaji wako ni mkubwa, basi unaweza kumwajiri mtu aliye na taaluma ya
utunzaji na usimamizi wa pesa.
Unaweza pia kujifunza wewe mwenyewe jinsi ya kutunza na
kutumia pesa vyema; unaweza pia kutumia programu za bure za kompyuta kama vile
Wave app kutunza mahesabu yako.
7. Usikate tamaa
Ni wazi kuwa katika safari ya ujasiriamali utakutana na
changamoto mbalimbali. Jambo la msingi ni kukumbuka kanuni hii kuwa usikate
tamaa.
Tumia changamoto kama chachu ya kukuhamasisha kufanya bidii
zaidi na usirudi nyuma.
Changamoto zipo leo na kesho lakini keshokutwa hazitakuwepo
tena; jambo unalotakiwa kufanya ni kutazama lengo lako na kufanya bidii kila
kukikucha kuzikabili changamoto husika ili ufikie lengo lako.
Hitimisho
Naamini umefahamu kuwa kuna kanuni muhimu ambazo wewe kama
mjasiriamali unatakiwa kuzizingatia ili uweze kufanikiwa. Ni wazi kuwa bidii,
mipango mizuri na kutokukata tamaa kutakuwezesha kufikia lengo lako la
kufanikiwa kama mjasiriamali.
Je una swali, maoni au changamoto ambayo ungependa
kutushirikisha? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini nasi tutafurahi
kukuhudumia. Pia unaweza kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook pamoja na
kuwashirikisha wengine makala hii.
Kwa maoni zaid unaweza kutucheki
ReplyDeleteSafi Sana'a kwa kuthubutuuu
DeleteShukrani ndugu
DeleteAhsante sana kwa somo zuri na muhimu.
ReplyDelete